News
Dkt Samia: Vijana wanufaike na uwekezaji katika mawasiliano
News
Wanawake 142 waanza mafunzo ya Female Future Programme Dar es Salaam
Na Mwandishi wetu, News info
Zaidi ya wanawake 142 wamepokelewa rasmi kushiriki toleo la 12 la programu ya mafunzo ya uongozi kwa wanawake, Female Future Programme (FFP), iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mafunzo hayo ya kiutendaji yameandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na Taasisi ya Usimamizi ya Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI).
Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba-Doran amesema programu hiyo imekuwa na mchango mkubwa kwa zaidi ya wanawake 800 waliokwisha pata mafunzo kwa zaidi ya muongo mmoja, na sasa inaendeshwa katika nchi sita kwa ufadhili wa NHO, huku akiwahamasisha washiriki kushiriki kikamilifu safari ya miezi tisa ya mafunzo. Aidha, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ESAMI, Dkt. David Kalaba amesema jamii inahitaji wanawake viongozi wenye kujiamini na uwezo mkubwa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya haraka, akisisitiza umuhimu wa mtazamo wa kimataifa, kujifunza na kuendana na mabadiliko pamoja na uwezo wa kusimamia utofauti, kutatua migogoro na kutoa thamani kwa wateja.
Kwa upande wake, Meneja wa Upstream wa IFC, Bw. Sam Nganga aliyemwakilisha Meneja wa Nchi, Bi. Martine Valcin amesema taasisi hiyo inaendelea kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi katika ngazi za juu za uongozi ili kukuza ushirikishwaji, huku akiwahimiza washiriki kujisimamia na kutumia kikamilifu mafunzo hayo.
Katika hafla hiyo pia kulikuwa na mjadala wa jopo kuhusu wanawake katika uongozi uliowashirikisha wataalamu mbalimbali wa rasilimali watu na uongozi kutoka taasisi tofauti, ambapo ilisisitizwa kuwa kuchanganya uzoefu wa vizazi tofauti vya wanawake kazini huleta matokeo chanya pamoja na umuhimu wa kujifunza ujuzi mpya na kuimarisha mentorship baada ya mafunzo.
Washiriki wa kundi la 12 walihimizwa kujenga mitandao imara ya kitaaluma, huku taasisi na makampuni yakitakiwa kutambua upekee wa kila mwanamke badala ya kuwaona kama kundi moja.
Akihitimisha, Mjumbe wa Bodi ya ATE, Bw. Gasper Kikui amesema sekta isiyo rasmi bado ina changamoto nyingi za uongozi na kuwataka washiriki kuyachukulia mafunzo hayo kwa uzito ili kuleta mabadiliko chanya.





News
Dkt Samia azindua minara 758, kuwanufaisha zaidi ya wananchi milioni nane
Na Mwandishi wetu, News info
Zaidi ya wananchi milioni 8.5 hususan wanaoishi mipakani na vijijini, wanatarajiwa kuondolewa changamoto ya mtandao, baada ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kuzindua minara 758 ya mawasiliano iliyojengwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Uzinduzi huo umefanyika leo Ijumaa Aprili 10, 2026 jijini Dodoma, ukiambatana na kuunganisha huduma za mkongo wa Taifa wa mawasiliano katika Wilaya 85, ikiwa ni juhudi za Serikali kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuongeza huduma za mawasiliano.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt Samia amesema uwekezaji huo umetokana na ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta ya mawasiliano ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi kwa ubora unaokidhi mahitaji ya teknolojia ya kisasa na kwa gharama nafuu.
Amesema kukamilika kwa ujenzi wa minara hiyo kutachochea ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kidijitali na kufungua fursa mpya za ajira, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya Taifa.
“Mawasiliano si tena huduma ya anasa kama ilivyokuwa zamani. Leo hii ni uti wa mgongo wa uchumi wa kisasa na daraja la fursa kwa wananchi katika nyanja mbalimbali za maendeleo,” amesema

News
Moduli Ya Rufaa Kuboresha Mnyororo Wa Ugavi
Na Mwandishi wetu, News info
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imesema ujenzi wa moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST utachangia kuongeza uwajibikaji, uwazi na ufanisi kwenye mnyororo wa ugavi.
Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando amebainisha hayo wakati wa uzinduzi rasmi wa Sera Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 na kuongeza kuwa Moduli hiyo imewaunganisha wazabuni wote na Taasisi nunuzi nchini ili kuongeza uwajibikaji katika utatuzi wa migogoro inayotokana na michakato ya ununuzi wa umma.
“PPAA ni moja kati ya taasisi zinazosimamia ununuzi wa umma nchini, matumizi ya moduli hiyo katika mnyororo wa ugavi yatachangia kutoa maamuzi kwa haki na wakati na kuwezesha miradi ya Serikali kutekelezwa kwa wakati uliokusudiwa,” amesema Bw. Sando.
Pamoja na mambo mengine, Bw. Sando amebainisha kuwa matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika ununuzi wa umma yatasaidia kuongeza uwazi, kupunguza gharama, kuokoa muda, utunzaji wa nyaraka na hivyo kuongeza ufanisi katika hukumu zinazotolewa kutokana na michakato mbalimbali ya zabuni za umma.
Bw. Sando ameongeza kuwa, PPAA imefanikiwa kushiriki katika utungwaji wa Sera ya Taifa ya Mnyororo wa Ugavi, Sheria ya Ununuzi wa Umma, Kanunuzi za Ununuzi wa Umma na Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma ambapo yote ni michango wa Mamlaka ya Rufani katika mnyororo wa ugavi.
Kadhalika, Mamlaka ya Rufani inatarajia kuboresha kipengele cha makundi maalum na vijana ambapo inategemea kuboresha gharama au tozo za kesi kwa makundi maalum pamoja na kuelekeza nguvu kwa vijana na kuhakikisha wanapata fursa ya kudai haki zao katika michakato ya ununuzi wa umma.
Awali akizindua Sera Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), amezielekeza mamlaka, taasisi na wadau wote wanaosimamia utekelezaji wa Sera hiyo kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, uwazi na utawala wa sheria.
Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo wakati akizundua Sera hiyo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Dkt. Nchemba amesema changamoto zinazoikumba sekta ya ununuzi wa umma hazitokani na sera au sheria zilizopo, bali ni uzembe na mitazamo ya baadhi ya watendaji.
Ameongeza kuwa taarifa za ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) zinaonesha wazi kuwa kasoro nyingi zinasababishwa na utekelezaji dhaifu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
“Sehemu kubwa ya changamoto hizo zinatokana na hulka, tabia na mitazamo ya watendaji. Hivyo, ni lazima tubadilike ili kufikia malengo ya sera hii,” amesisitiza Dkt. Mwigulu.
Aidha, Waziri Mkuu, amezitaka wizara, taasisi na mamlaka zote kufanya mapitio ya sera, sheria na kanuni zinazokinzana na sera hiyo ili kuweka mazingira rafiki ya utekelezaji wake.
Naye Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amesema sera hiyo ni mwongozo muhimu utakaosaidia kuimarisha mifumo ya ugavi katika sekta ya umma, kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na kudhibiti vitendo vya rushwa.
Balozi Khamis ameongeza kuwa utekelezaji wa sera hiyo utaongeza ajira, kuimarisha mnyororo wa thamani na kuchochea mageuzi makubwa ya kiuchumi kuelekea dira ya maendeleo ya mwaka 2050.




-
News8 months agoSABASABA AONGOZA CUSTOMER FORUM DODOMA
-
News11 months agoRais Samia apeleka Bilioni 669 za Barabara, Madaraja mikoa ya Kusini
-
Uncategorized11 months agoNMB Yaandika Historia kwa Kushinda Tuzo Sita Kubwa, Ikiwemo ya “Benki Bora kwa Uendelevu Barani Afrika”
-
News10 months agoFCC YATOA SEMINA YA MASUALA YA UHIBITI BANDIA KWA WAJASIRIAMALI WANAWAKE
-
Uncategorized11 months agoNMB Foundation yawanoa Wakulima wa Zao la Kakao Kyela, Serikali yaipongeza
-
News8 months agoTRA, NCAA, TANAPA na TAWA Kuunda Kamati Tendaji ya Pamoja Kuongeza Mapato
-
News10 months agoRais Mwinyi aizawadia Yanga Milioni 100
-
News11 months agoDkt. Biteko akutana na Mtendaji Mkuu wa PUMA Duniani

