Connect with us

News

Rais Samia apeleka Bilioni 669 za Barabara, Madaraja mikoa ya Kusini

Published

on

Na Mwandishi wetu, NewsInfo Online

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametangaza kuwa Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan itatumia kiasi cha Shilingi Bilioni 669 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwa lengo la kuboresha usafiri na kuifungua mikoa hiyo kiuchumi.

Akizungumza mkoani Mtwara, Ulega alisema barabara na madaraja hayo yatajengwa kupitia barabara za Mtwara –Mingoyo (Mnazi mmoja)-Masasi (km 201) itakayogharimu kiasi cha shilingi bilioni 401 huku barabara nyingine ya Mtwara Tandahimba-Newala-Masasi itagharimu kiasi cha shilingi bilioni 268 hadi kukamilika kwake.

Waziri Ulega amewaambia wananchi wa Mtwara kwamba kiasi hicho kikubwa cha fedha katika ujenzi wa miundombinu hiyo unaonyesha dhamira ya dhati aliyonayo Rais Samia kwa wananchi wa Mikoa ya Kusini na lengo kubwa ni kuhakikisha inafunguka kiuchumi na kuwapa wananchi fursa za kiuchumi.

“Wananchi wa mikoa ya Kusini, ninawaletea salamu hizi za Rais wenu Samia Suluhu Hassan. Hizi barabara zikikamilika kutakuwa na taa za barabarani takribani 4800 kutoka Mtwara hadi Masasi. Kusini kutang’ara kwa mwanga nyakati za usiku na kutapendeza. Kwenye barabara nzuri, uchumi unafunguka na kwenye mwanga kwa saa 24, biashara zinafanyika muda wote,”alisema Ulega.

Ulega yuko katika ziara ya kikazi mkoani Mtwara ambapo pamoja na mambo mengine anafuatilia maagizo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuangalia maendeleo ya ukarabati wa barabara na miundombinu mingine ya ujenzi iliyoharibiwa wakati wa mvua za masika na kimbunga cha Hidaya kuanzia mwishoni mwa mwaka jana hadi mwaka huu.

Akitoa mchanganuo, Ulega alisema katika kiasi hicho cha fedha, zaidi ya shilingi bilioni 230 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mnivata – Newala – Masasi (km 160) kwa kiwango cha lami pamoja na Daraja la Mwiti (m 84) ili kuzifungua Wilaya za Masasi, Newala, Tandahimba na Mtwara kiuchumi kupitia usafirishaji wa abiria na mazao.

Ulega amewataka Makandarasi wanaojenga barabara ya Mnivata-Masasi kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi wazawa wa maeneo barabara inakopita kwa kushirikisha ofisi za Serikali za Mtaa na Kata za Wilaya.

Amesisitiza kuwa licha ya Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara, miradi hiyo inapaswa kuzalisha ajira kwa wananchi wazawa na kuacha ujuzi ili uweze kuwasaidia katika majukumu mengine ya kijamii na kiuchumi.

Ulega ameitaka TANROADS kukamilisha taratibu za kuwapata wakandarasi watakaotekeleza miradi Jumuishi ya kijamii (CSR) ili ujenzi wa barabara uende sambamba na miradi hiyo ambayo itahusisha ujenzi wa Kituo cha Mabasi, ghala, ununuzi wa mashine za kubangulia korosho, mabweni ya shule, nyumba za madaktari, ununuzi wa X-Ray na gari la wagonjwa.

Naye, Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Dotto John ameeleza mradi huo unaotekelezwa na Mkandarasi China WuYi umegawanywa katika sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza ya Mnivata – Mitesa (km 100) unatekelezwa kwa muda wa miezi 36 na sehemu ya pili ya Mitesa – Masasi (km 60) na ujenzi wa Daraja la Mwiti (m 84) unatekelezwa kwa muda wa miezi 30.

Kwa upande wake, Mbunge wa Tandahimba Ahmad Katani ameishukuru Serikali kwa mradi wa barabara hiyo kwani ni barabara ya kiuchumi kwa kuwa inapita katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa Korosho.

Continue Reading
Click to comment
0 0 votes
Article Rating
Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments

News

Wanawake 142 waanza mafunzo ya Female Future Programme Dar es Salaam

Published

on

By

Na Mwandishi wetu, News info

Zaidi ya wanawake 142 wamepokelewa rasmi kushiriki toleo la 12 la programu ya mafunzo ya uongozi kwa wanawake, Female Future Programme (FFP), iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Mafunzo hayo ya kiutendaji yameandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na Taasisi ya Usimamizi ya Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI).

Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba-Doran amesema programu hiyo imekuwa na mchango mkubwa kwa zaidi ya wanawake 800 waliokwisha pata mafunzo kwa zaidi ya muongo mmoja, na sasa inaendeshwa katika nchi sita kwa ufadhili wa NHO, huku akiwahamasisha washiriki kushiriki kikamilifu safari ya miezi tisa ya mafunzo. Aidha, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ESAMI, Dkt. David Kalaba amesema jamii inahitaji wanawake viongozi wenye kujiamini na uwezo mkubwa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya haraka, akisisitiza umuhimu wa mtazamo wa kimataifa, kujifunza na kuendana na mabadiliko pamoja na uwezo wa kusimamia utofauti, kutatua migogoro na kutoa thamani kwa wateja.

Kwa upande wake, Meneja wa Upstream wa IFC, Bw. Sam Nganga aliyemwakilisha Meneja wa Nchi, Bi. Martine Valcin amesema taasisi hiyo inaendelea kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi katika ngazi za juu za uongozi ili kukuza ushirikishwaji, huku akiwahimiza washiriki kujisimamia na kutumia kikamilifu mafunzo hayo.

Katika hafla hiyo pia kulikuwa na mjadala wa jopo kuhusu wanawake katika uongozi uliowashirikisha wataalamu mbalimbali wa rasilimali watu na uongozi kutoka taasisi tofauti, ambapo ilisisitizwa kuwa kuchanganya uzoefu wa vizazi tofauti vya wanawake kazini huleta matokeo chanya pamoja na umuhimu wa kujifunza ujuzi mpya na kuimarisha mentorship baada ya mafunzo.

Washiriki wa kundi la 12 walihimizwa kujenga mitandao imara ya kitaaluma, huku taasisi na makampuni yakitakiwa kutambua upekee wa kila mwanamke badala ya kuwaona kama kundi moja.

Akihitimisha, Mjumbe wa Bodi ya ATE, Bw. Gasper Kikui amesema sekta isiyo rasmi bado ina changamoto nyingi za uongozi na kuwataka washiriki kuyachukulia mafunzo hayo kwa uzito ili kuleta mabadiliko chanya.

Continue Reading

News

Dkt Samia: Vijana wanufaike na uwekezaji katika mawasiliano

Published

on

By

Na Mwandishi wetu, News info

Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, ametaka vijana wanufaike ipasavyo na huduma za mkongo wa Taifa wa mawasiliano, hasa katika maeneo ya kukuza ubunifu, ujuzi wa kidigitali na fursa za ajira.

Ametaka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, zishirikiane na wadau wa sekta ya teknolojia ili vijana wapate manufaa hayo.

Dkt Samia ameyasema hayo leo, Ijumaa Aprili 10, 2026 jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi huo, ukiambatana na kuunganisha huduma za mkongo wa Taifa wa mawasiliano katika Wilaya 85.

“Uwekezaji huu kwa vijana ni muhimu kwa sababu dunia ya teknolojia ni ya kwao. Dunia hii ipo viganjani mwao na ndiyo mfumo wa maisha yao. Ni lazima tuwawezeshe na kuwahamasisha kutumia mifumo hii ili waweze kukua kiuchumi na kijamii,” amesema.

Continue Reading

News

Dkt Samia azindua minara 758, kuwanufaisha zaidi ya wananchi milioni nane

Published

on

By

Na Mwandishi wetu, News info

Zaidi ya wananchi milioni 8.5 hususan wanaoishi mipakani na vijijini, wanatarajiwa kuondolewa changamoto ya mtandao, baada ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kuzindua minara 758 ya mawasiliano iliyojengwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Uzinduzi huo umefanyika leo Ijumaa Aprili 10, 2026 jijini Dodoma, ukiambatana na kuunganisha huduma za mkongo wa Taifa wa mawasiliano katika Wilaya 85, ikiwa ni juhudi za Serikali kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuongeza huduma za mawasiliano.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt Samia amesema uwekezaji huo umetokana na ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta ya mawasiliano ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi kwa ubora unaokidhi mahitaji ya teknolojia ya kisasa na kwa gharama nafuu.

Amesema kukamilika kwa ujenzi wa minara hiyo kutachochea ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kidijitali na kufungua fursa mpya za ajira, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya Taifa.

“Mawasiliano si tena huduma ya anasa kama ilivyokuwa zamani. Leo hii ni uti wa mgongo wa uchumi wa kisasa na daraja la fursa kwa wananchi katika nyanja mbalimbali za maendeleo,” amesema

Continue Reading

Trending

Copyright © 2025 Newsinfo.