News
Dkt Samia: Kodi zisipendelee wala kukandamiza watu
Na Mwandishi wetu, News Info Online
Rais wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan amesema mapendekezo ya Tume aliyoiunda ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi, yanashauri kuwepo kwa utulivu katika ulipaji wa kodi wafanyabiashara.
Mkuu huyo wa nchi, amefafanua kuwa Tume hiyo inapendekeza sera za ulipaji wa kodi ziwe zimetulia na zinazotekelezeka, sambamba na kuwa na tafsiri moja ya kisheria inayoeleweka.
“Sio sheria ambazo mfanyabiashara akisoma kifungu hicho hicho anauelewa tofauti na mkusanyaji wa mapato akisoma kifungu hicho hicho anauelewa tofauti. Tuwe na sheria ambayo kifungu kinachosema kisimame hivyo hivyo kwa mfanyabiashara na mkusanyaji wa kodi,” ameeleza Dkt Samia.
Rais Dkt Samia ameeleza hayo leo Jumatano Machi 18,2026 wakati akipokea ripoti ya Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi nchini, hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Lakini kwa upande mwingine kodi zetu ziwe ‘neutral’ hazikandamizi watu wala kupendelea watu. Ziwe neutral mfanyabiashara afanye shughuli zake, alipe kodi na Serikali ikusanye mapato,” amesema nakuongeza kuwa:
“Pia zisiumize wale ambao wale ambao… lakini ziwe kodi zinazokuza biashara na mapato nchini. Lakini jingine kodi zitutoshe na kuendelea kuongeza wigo wa ukusanyaji,” ameeleza Dkt Samia.
