News
FCC YATOA SEMINA YA MASUALA YA UHIBITI BANDIA KWA WAJASIRIAMALI WANAWAKE
Na Mwandishi wetu, Newsinfo Online
Tume ya Ushindani (FCC) imeendesha semina maalum ya Uhamasishaji wa masuala ya ushindani, kumlinda mlaji na udhibiti wa Bidhaa bandia kwa wanawake wajasiriamali Mkoa wa Dar es Salaam, kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo Sheria zinazosimamia masuala ya Ushindani nchini.
Semina hiyo ya siku moja imefanyika June 13, 2025 katika Ofisi za FCC Jijini Dar es Salaa, kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC), ili kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) kuelewa zaidi sheria na kanuni za ushindani wa haki zitakazosaidia kufanya shughuli zao kwa weledi.
Akizungumza alipokuwa akifungua kikao hicho, kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC Bi. Khadija Ngasongwa, Mkurugenzi wa Tafiti, Muungano wa Makampuni na Uraghibishi Bi. Zaytun Kikula, amesema mafunzo hayo yana mchango mkubwa katika kuimarisha mazingira ya Biashara nchini.
“Jukwaa hili linaturuhusu kushirikiana moja kwa moja na wamiliki wa biashara, kuwaelimisha juu ya sheria za ushindani, na kuhakikisha wanajenga biashara imara na endelevu,” alisema.

Aidha, Bi. Kikula amesema anaamini kuwa wafanyabiashara wanawake wana nafasi kubwa katika maendeleo ya kiuchumi, ustawi wa familia na ukuaji wa jamii, nakwamba utowawezesha kuna athari ya moja kwa moja kwa jamii.
Amesisitiza kuwa kulinda biashara dhidi ya ushindani usio wa haki, pamoja na kuhakikisha wateja wanapokea bidhaa na huduma bora, inasalia kuwa sehemu ya msingi ya mamlaka ya FCC.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa TWCC Bi. Mwalongo Kambewe amewataka washiriki kutumia mafunzo waliyoyapata kuimarisha shuguli zao, huku akibainisha kuwa maarifa huleta mabadiliko
Kila unapojifunza unakua” Bi. Kambewe amesema na kuongeza kuwa “Ninaamini wanawake hawa wataona mabadiliko sio tu katika biashara zao bali hata katika familia na jamii zao. amesema.
Naye Kaimu Meneja wa Makubaliano ya Washindani wa FCC, Bw. David Mawi, akizungumza alipokuwa akitoa wasilisho katika semina hiyo, amesisitiza kuwa soko huria haliwezi kuendelea bila kuwepo udhibiti.
“Soko huria haliwezi kuendelea bila mdhibiti, Tunahitaji kulinda biashara na watumiaji dhidi ya mazoea yasiyo ya haki ambayo mara nyingi yanalenga washiriki wadogo au wapya kwenye soko.” Amesema Bw. Mawi
Ameongeza kuwa kutumia vibaya utawala wa soko, unaofafanuliwa kama kudhibiti zaidi ya asilimia 40 ya hisa ya soko kwa muda endelevu, ni ukiukaji wa sheria na hatari ya kuwadhuru washindani na watumiaji.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za FCC katika kuhakikisha wajasiriamali wanawake wa Kitanzania wanapata maarifa na kujengewa uelewa ili kufanikiwa katika soko la ushindani, ndani na nje ya nchi.