News
Makonda amsifu Dkt. Samia kwa uwezo wa kuhimili changamoto za taifa
Na Mwandishi wetu, NewsInfo – Arusha
Mgombea Ubunge Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Paul Makonda, amemuombea kura Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na uthubutu na uongozi wake imara unaoonyesha uwezo mkubwa wa kuliongoza taifa katika nyakati ngumu.
Akizungumza na wananchi Mkoani Arusha, katika mtaa wa Majengo ya Juu, Makonda alisema katika maisha ya uongozi, kila kiongozi hupimwa kwa matendo yake hasa katika kipindi kigumu ambacho taifa linapitia, na kwamba Dkt. Samia amethibitisha kuwa na uwezo wa kuhimili changamoto na kulipeleka taifa katika mwelekeo sahihi.
“Moja ya sifa kubwa ya kiongozi inayomtofautisha na wengine ni uwezo wake wa kukabiliana na changamoto zinazoweza kulikumba taifa na kulibakisha salama,” alisema Makonda.
Aliongeza kuwa mataifa mengi Duniani yamejikuta yakitumbukia katika migogoro na vita kama ilivyotokea kati ya Ukraine na Urusi, lakini chini ya uongozi wa Dkt. Samia, Tanzania imeendelea kubaki nchi yenye amani na umoja.
Makonda alisisitiza kuwa Dkt. Samia ameonyesha kwa vitendo uwezo wa kukabiliana na changamoto ambazo zingesababisha mgawanyiko wa kitaifa, na badala yake ameendeleza misingi ya umoja na mshikamano iliyowekwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
