News
Makonda kuleta neema kwa vijana
Na Mwandishi wetu, NewsInfo – Arusha
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, amesema atahakikisha vijana wanapatiwa fursa mbalimbali za kiuchumi ili waweze kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Akizungumza wakati alipokuwa akipita mtaa kwa mtaa kuhamasisha wananchi kupiga kura siku ya Tarehe 29 Oktoba, Makonda alisema serikali itawajengea uwezo vijana kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kupunguza changamoto za ajira.
“Tutahakikisha tunamuwezesha kijana afanye majukumu yake vizuri. Vijana wapo wanaofanya kazi kwa ajili ya hali ngumu ya maisha, tutahakikisha tunaibua fursa za kiuchumi ili kila kijana awe na shughuli za kufanya,” alisema Makonda.
Aidha, alisisitiza kuwa usalama wa nchi ni jukumu la wananchi wote, akihimiza jamii kushirikiana katika kuwalinda watoto na kuhakikisha maeneo wanayoishi yanakuwa salama.
“Watoto wanaofanya matukio ni watoto wetu, kila mmoja anatakiwa kuwa sehemu ya ulinzi wa watoto kuanzia ngazi za familia,” aliongeza.
Makonda pia alisema watahakikisha thamani ya mabalozi na ngazi za mashina inarejeshwa, ili wawe walinzi wa ulinzi na usalama katika maeneo yao chini ya usimamizi wa wenyeviti wa mitaa na vijiji kuhakikisha kila kaya inakuwa salama.
Akizungumzia mikopo, alisema ndani ya halmashauri kuna aina nne za mikopo inayotokana na makusanyo ya mapato ya ndani ambayo ni kwa wanawake, vijana, vikundi maalum (special groups) na kupitia ofisi mbalimbali za serikali kama Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Ofisi ya Waziri Mkuu na mikopo ya uwezeshaji kiuchumi. Aliahidi kuhakikisha wananchi wanaelewa taratibu za mikopo hiyo na kuipata kwa urahisi.
Kuhusu kupanda kwa bei ya gesi za kupikia, Makonda alisema Tanzania bado haijafikia kiwango cha uzalishaji wa kutosha kwani gesi nyingi zinaagizwa kutoka nje ya nchi, huku matumizi yake yakiongezeka zaidi ya uzalishaji wa ndani.
Vilevile, Makonda alisema jiji la Arusha bado lipo nyuma katika miundombinu ya barabara, hivyo atahakikisha miundombinu hiyo inaboreshwa ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.
Akihitimisha, Makonda aliwakumbusha wananchi kuwa tarehe 29 Oktoba ni siku muhimu ya kupiga kura, akiwataka wajitokeze kwa wingi kushiriki katika zoezi hilo.
“Tarehe 29 ndiyo siku ya kupiga kura. Twende tukaombe kura kwa Dkt. Samia, wabunge na madiwani wetu. Vituo vimesogezwa karibu na makazi yetu jumla ya vituo 1,051 katika Jimbo la Arusha,” alisema Makonda.
Aliongeza kuwa kampeni yao ni ya mlango kwa mlango, wakihamasisha wananchi wote kujitokeza.
“Wanaokuja hapa ni wakazi wa jiji la Arusha, na wengine siyo wakazi wa jiji hili. Usisahau kuwaombea kura pia madiwani wa huko na Dkt. Samia. Ukikutana na bodaboda, mtu wa hoteli, au mfanyabiashara msemeshe, tuwahimize wote kujitokeza kupiga kura Oktoba 29,” alisisitiza.
Makonda pia aliwahimiza wale waliopoteza vitambulisho vya kupigia kura wasikate tamaa.
“Kuna wengine wamepoteza vitambulisho vyao. Chukua kile chenye majina yanayofanana na yale uliyotumia kujiandikisha. Ukifika kituoni utamuona msaidizi atakayekusaidia. Muhimu ni kushiriki kwenye kura hii ya kihistoria,” alihitimisha.
