News

Makonda tunakwenda kuchechemua uchumi wa Arusha kwa kuwekeza kwenye miundombinu na Ajira

Published

on

Na Mwandishi wetu, NewsInfo – Arusha

Mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, amesema dhamira yake ni kuhakikisha Arusha inakuwa kitovu cha uchumi kwa kuwekeza kwenye maeneo ya viwanda, miundombinu, huduma bora kwa wananchi na ujenzi wa mazingira rafiki ya kiuchumi.

Akizungumza na wananchi wa Arusha, Makonda alisema kuwa eneo la viwanda ndilo linalotoa fursa kubwa ya ajira na kuinua kipato cha wananchi, hivyo Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kulipa kipaumbele kwa kujenga viwanja vya AFCON, kumbi za mikutano na maeneo ya uwekezaji ambayo yote yanalenga kuleta wageni, kuongeza mzunguko wa fedha na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Arusha.

Makonda aliongeza kuwa eneo la pili lenye umuhimu mkubwa ni miundombinu, ikiwemo maji, shule, afya, barabara na kumbi mbalimbali. Alisema ujenzi wa miundombinu imara ni nguzo ya maendeleo na ndio msingi wa uchumi endelevu.

“Juzi nilikwenda kuangalia Bandari ya Dar es Salaam, Rais Samia amewekeza kwa kiwango kikubwa. Tumeona mizigo ikiongezeka kutoka tani milioni 18 hadi milioni 27 kwa mwaka. Siyo tu bandari ya Dar es Salaam, bali pia Mtwara imeongezeka kutoka tani 590,000 hadi milioni 2.59, na Tanga kutoka tani 830,000 hadi milioni 1.3. Hii inaonesha namna uwekezaji unavyokuza uchumi,” alisema Makonda.

Ameeleza kuwa katika miaka mitano ijayo, ataweka mkazo katika kuboresha huduma kwa wananchi kwa kuzingatia kaulimbiu ya mgombea urais wa CCM, “Kazi na Utu.”

“Kazi ni ile inayojenga uchumi na kuboresha mazingira, lakini utu ni kumthamini kila mtu kwa heshima bila kujali kipato chake,” alisema Makonda.

Aidha, Makonda aliahidi kuwa Jimbo la Arusha Mjini litakuwa namba moja kwa watu kupata haki zao, akisema hataki kuona wanawake wakinyanyasika wanapofika hospitalini au wananchi wanapokwenda kwenye serikali za mitaa na vituo vya polisi.

“Hatutambagua mtu. Tutahakikisha kila mmoja anaheshimika, anapata haki yake na kutimiza wajibu wake. Hiyo ndiyo ndoto yetu,” alisisitiza.

Makonda alisema awamu inayofuata ya miaka mitano itakuwa ni ya kuuchechemua uchumi wa Arusha, kuhakikisha kila eneo lenye fursa ya kiuchumi linatumiwa vizuri ili wananchi wa Arusha wawe na kipato cha uhakika.

Akiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi tarehe 29 kupiga kura, Makonda alisema ni muhimu kumchagua kiongozi mwenye uwezo, busara na uzoefu wa kulinda uchumi, diplomasia na usalama wa nchi kama alivyoonyesha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Tulipopoteza Rais, taifa halikugawanyika kwa sababu tulikuwa na mwanamama mwenye maono makubwa na utulivu wa hali ya juu. Tumepita salama kwa uimara wake,” alisema.

Akizungumzia maandamano yanayotangazwa na baadhi ya watu mitandaoni, Makonda alisema taarifa alizonazo zinaonyesha kwamba waliohusika walikuwa wakitafuta fedha, na sasa wamekwisha kukosa ufadhili.

“Niliwaambia watu Kariakoo, mtu akikushawishi uache kazi yako ukaandamane, mwambie aniambie kwanza nipe pesa yangu kabla sijaacha kazi ninayoniingizia kipato,” alisema Makonda.

Alimalizia kwa kusema kuwa wananchi wa Arusha wanapaswa kuchagua maendeleo, umoja na ustawi wa watu kupitia kazi na utu, si maneno ya mitandaoni.

0 0 votes
Article Rating
Subscribe
Notify of
0 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments

Trending

Exit mobile version