News

MIXX, TCCIA NA YAS BUSINESS WAUNGANA KUHARAKISHA MAPINDUZI YA MALIPO KIDIJITALI TANZANIA

Published

on

Na Mwandishi wetu, NewsInfo Online

Kampuni ya huduma za kifedha kwa njia ya simu Mixx imeingia makubaliano ya ushirikiano na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) pamoja na Yas Business, kwa lengo la kuimarisha malipo ya kisasa na kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini.

Makubaliano hayo yanalenga kuwaunganisha wafanyabiashara, wakulima, wanawake na vijana katika uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Angelica Pesha, alisema hatua hiyo itachochea ajenda ya taifa ya uchumi wa viwanda na kusaidia kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

“Kupitia huduma za Mixx na ushirikiano na Yas Business, wanachama wa TCCIA watawezeshwa kupata suluhisho za malipo kidijitali, mawasiliano ya kisasa na elimu ya kifedha. Ushirikiano huu hautabaki kwenye makaratasi bali utatafsirika katika miradi ya vitendo itakayogusa kila mwanachama wa TCCIA na wananchi kwa ujumla,” alisema Pesha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA, Bw. Oscar Kissanga, alieleza kuwa ushirikiano huo unakuja wakati muafaka ambapo wafanyabiashara na wakulima wadogo wanakabiliwa na changamoto za mitaji, upatikanaji wa taarifa za masoko na huduma za kifedha za kisasa.

“Sekta binafsi na wabunifu wa teknolojia kama Mixx na Yas Business ni wadau muhimu katika safari ya kuelekea uchumi wa kipato cha kati na hatimaye kipato cha juu. Ushirikiano huu unafungulia wanachama wetu milango ya huduma bora za kifedha na mawasiliano, hivyo kuwawezesha kushindana ndani na nje ya nchi,” alisema Kissanga.

Makubaliano hayo yamejikita katika maeneo matatu makuu:
1. Kuimarisha mifumo ya malipo ya kidijitali kwa wanachama wa TCCIA kupitia huduma bunifu za Mixx, ili kuongeza ufanisi, uwazi na usalama wa miamala.
2. Kutoa huduma za kisasa za intaneti na mawasiliano kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) kupitia Yas Business, ili kuongeza tija na upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati.
3. Kuwekeza katika elimu ya kifedha na ujuzi wa kidijitali kwa vijana na wanawake, ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa unaotegemea teknolojia.

Kupitia ushirikiano huu, taasisi husika zinatarajia kuchochea ukuaji wa biashara zenye ushindani, kupanua wigo wa ujumuishi wa kifedha, na kuweka msingi wa uchumi endelevu, shirikishi na wenye mnepo kwa Tanzania ya sasa na ya baadaye.

0 0 votes
Article Rating
Subscribe
Notify of
0 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments

Trending

Exit mobile version