News
NMB, PPRA waimarisha uhakiki wa dhamana za zabuni kidigitali
Na Mwandishi wetu, News Info Online
Imeelezwa kuwa huduma ya uhakiki wa dhamana za zabuni za kibenki kupitia mfumo wa NeST ni hatua muhimu ya kuimarisha uwazi, ufanisi na usalama katika michakato ya ununuzi wa umma nchini.
Akizungumza katika uzinduzi wa huduma ya uhakiki wa dhamana za zabuni za kibenki za Benki ya NMB kupitia mfumo wa NeST, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, alisema kuunganishwa kwa mfumo wa NeST na mifumo ya benki hiyo kutasaidia kuboresha mfumo wa ununuzi wa umma na kuwawezesha wafanyabiashara kushiriki zabuni kwa uwazi na haki.
“Kupitia mfumo huu, NMB itawezesha uhakiki wa Bank Guarantee pamoja na akaunti za waombaji zabuni na kutoa majibu papo hapo, jambo litakalorahisisha mchakato na kuongeza ufanisi kwa wataalamu wa ununuzi na ugavi,” amesema Zaipuna.
Ameongeza kuwa huduma ya Digital Bank Guarantee Confirmation itawawezesha wateja kuwasilisha na kuthibitisha dhamana za benki kama Bid Bond, Advance Guarantee na Performance Guarantee moja kwa moja kupitia mfumo wa NeST.
“Kupitia huduma hii ya kidijitali, wateja sasa wanaweza kuwasilisha na kuthibitisha dhamana za benki moja kwa moja kupitia mfumo wa NeST, jambo litakalopunguza muda wa kukamilisha taratibu za zabuni na kuondoa hatari ya udanganyifu,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, amesema mfumo huo utarahisisha michakato ya zabuni na kuondoa changamoto za uthibitishaji wa dhamana za kibenki.
“Kupitia mfumo wa NeST, taasisi nunuzi sasa zinaweza kuthibitisha dhamana za zabuni moja kwa moja kupitia mfumo bila kuwasiliana na benki husika, jambo ambalo linaongeza uwazi na ufanisi katika michakato ya ununuzi wa umma,” amesema Simba.
Ameeleza kuwa mzabuni ataweka namba ya dhamana aliyopewa na benki kwenye mfumo wa NeST, kisha mfumo huo utaivuta moja kwa moja kutoka benki husika na kuiwasilisha kwa taasisi nunuzi.
“Hatua hii imeondoa kabisa mianya ya kughushi nyaraka za dhamana za kibenki na pia inapunguza muda wa kuthibitisha uhalali wake,” amesema.
