News

NMB Yazindua Jukwaa la JASIRI Kukuza Uwezo wa Wanawake Kiuchumi

Published

on

Na Mwandishi wetu, News Info Online

Benki ya NMB imezindua jukwaa la JASIRI lenye lengo la kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia fursa za elimu ya fedha, huduma za kifedha, ushirikiano wa kibiashara pamoja na majukwaa ya kujifunza na kushirikiana katika kukuza biashara zao.

Uzinduzi huo umefanyika sambamba na maadhimisho ya Mwezi wa Wanawake Duniani ikiwa ni sehemu ya jitihada za benki hiyo kukuza uchumi jumuishi nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Bw. Filbert Mponzi, amesema jukwaa la JASIRI linaonesha dhamira ya benki hiyo katika kuwawezesha wanawake ambao wameendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa Tanzania.

“Takwimu zinaonesha kuwa wanawake wanamiliki au kuendesha karibu nusu ya biashara nchini, lakini bado wengi wao wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mitaji, mitandao ya biashara pamoja na fursa za kukuza biashara zao.”

Amesema kuwa NMB inaamini uwezeshaji wa wanawake hauishii katika utoaji wa huduma za kifedha pekee, bali pia ni kujenga mazingira yatakayowawezesha wanawake kuunganishwa, kujifunza na kushirikiana ili kufungua fursa zaidi za kukuza biashara na kutimiza ndoto zao.

Mponzi ameeleza kuwa kupitia jukwaa la JASIRI, wanawake watapata nafasi ya kushiriki katika mazungumzo ya ushirikiano yatakayosaidia kubuni fursa mbalimbali zinazohusisha elimu ya fedha, huduma za kifedha, ujasiriamali pamoja na ushirikiano wa kimkakati.

Ameongeza kuwa mpango huo umeimarishwa kupitia tafiti na tathmini zilizofanywa kwa kushirikiana na washirika wa NMB, IFC na Mastercard, ili kubuni suluhisho zinazokidhi mahitaji ya wanawake katika kukuza biashara zao.

“Kuwekeza katika suluhisho zinazowawezesha wanawake ni fursa muhimu kijamii na kiuchumi, kwani wanawake ni miongoni mwa makundi yanayokua kwa kasi katika ujasiriamali na pia ni wahusika wakuu katika maamuzi mengi ya kifedha ndani ya familia nyingi nchini.”

Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto katika upatikanaji wa mitaji, masoko na maarifa ya kifedha, huku akibainisha kuwa kwa mujibu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, kuna pengo la ufadhili linalokadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni 42 kila mwaka katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“NMB inaona fursa katika kusaidia kuziba pengo hilo kwa kubuni bidhaa, huduma na majukwaa yanayolenga mahitaji ya wanawake” amesema Mponzi na kuongeza kuwa;

“Wanawake wanapopata ujumuishaji wa kifedha wana uwezo mkubwa wa kukuza biashara zao, kuweka akiba zaidi, kuwekeza katika familia zao na kuchangia kujenga jamii imara na yenye ustahimilivu.”

Aidha, ametoa pongezi kwa wanawake wote wa Tanzania kwa mchango wao mkubwa katika familia, jamii na uchumi wa taifa, akisema benki hiyo itaendelea kuwaunga mkono kupitia huduma bora za kifedha, elimu pamoja na fursa mbalimbali zitakazowawezesha kukua na kufanikiwa.

Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Masoko ya Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Irene Mutigazi, amesema jukwaa la JASIRI ni wito kwa wanawake kuamini katika uwezo wao na kuthubutu kufuatilia ndoto zao.

Amesema kupitia jukwaa hilo pamoja na Kochi la Orange la JASIRI, wanawake wataalikwa kushiriki mazungumzo, kupata ushauri, elimu ya fedha na fursa mbalimbali za kukuza biashara zao ikiwa ni sehemu ya kampeni ya benki hiyo ya “Tuyajenge.”

Naye Meneja Mwandamizi wa Bidhaa za Amana wa NMB, Beatrice Mwambije, amesema kupitia jukwaa la JASIRI benki hiyo imeandaa suluhisho mbalimbali za kifedha zinazolenga kuwawezesha wanawake, ikiwemo mikopo ya biashara, mikopo ya kidigitali, mikopo ya vikundi pamoja na bidhaa za akiba.

Ameongeza kuwa sambamba na huduma hizo, wanawake watapatiwa mafunzo ya elimu ya fedha, ushauri wa biashara pamoja na fursa za kujenga mitandao ya kibiashara ili kuwasaidia kukuza biashara zao na kufikia uhuru wa kifedha.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa tatu kushoto) akiwa pamoja na wadau wa Jukwaa Maalum la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi liitwalo NMB Mwanamke Jasiri baada ya uzinduzi uliofanyika jijini Dar es Salaam Machi 12 2026. Wengine ni Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC), Louise Gardiner (wa pili kushoto), Mwakilishi Mkazi wa MasterCard Tanzania Moses Alphonse ( kulia), Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi (kushoto), Mtangazaji wa radio, Najma Paul (wa tatu kulia) na Mwakilishi wa IFC, Joy Kemibaro (wa pili kulia).

0 0 votes
Article Rating
Subscribe
Notify of
0 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments

Trending

Exit mobile version