News

Prof. Mkumbo: Vijana wengi bado wamekwama katika fikra za zamani za kutegemea ajira Serikalini

Published

on

Na Mwandishi wetu, News Info Online

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema vijana wengi bado wamekwama katika fikra za zamani za kutegemea ajira serikalini, akisisitiza kuwa hali hiyo ndiyo chanzo cha kukua kwa tatizo la ukosefu wa ajira kwa wahitimu nchini.

Prof. Mkumbo amesema zama za kuhitimu chuo na kuajiriwa serikalini mara moja ‘zimepitwa na wakati’, na kusisitiza kuwa serikali inachukua hatua mahsusi za kulivunja tatizo hilo kwa kuongeza uwezo wa vijana kujiajiri, kuwekeza na kuajiri wenzao.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam siku ya Jumatatu, Waziri Mkumbo amesema changamoto ya ajira kwa wahitimu inagusa bara zima la Afrika, na Tanzania haiwezi kuendelea kuendeleza mfumo wa kutegemea serikali kuwa mwajiri mkuu wakati nafasi zake ni chache sana na haziwezi kupokea kila mhitimu wa vyuo vikuu na vyuo vya ufundi. Amesema njia pekee ni kuhakikisha sekta binafsi inapanuka na vijana wenyewe kuwa sehemu ya injini ya ajira nchini.

Miongoni mwa hatua ambazo serikali itazichukua ni kuanzisha Kituo Maalum cha Kuhudumia na Kuwezesha Wawekezaji Vijana (Youth Investors Resource Centre). Kituo hicho kitatoa mafunzo, usaidizi wa uwezeshaji na huduma mbalimbali kwa vijana wanaotaka kuwekeza. Kitakuwa Mabibo, Dar es Salaam, huku kukiwa na uwakilishi katika ofisi za TISEZA za mikoa na kanda. Waziri amesema anatarajia kukizindua kituo hicho kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Aidha Prof. Kitila amesema Serikali inaanzisha programu maalum ya kuwezesha vijana kubuni na kuanzisha uwekezaji wa viwanda katika maeneo mbalimbali nchini. Katika mpango huo, maeneo maalum yametengwa kwa ajili ya vijana waliomaliza vyuo vikuu na vyuo vya ufundi ili waweze kuwekeza.

0 0 votes
Article Rating
Subscribe
Notify of
0 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments

Trending

Exit mobile version