News

Rais Samia asifiwa kwa uwekezaji wa kisasa kwenye mradi wa SGR

Published

on

Na Mwandishi wetu, NewsInfo – Arusha

Mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, amemsifia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji bora wa mradi wa Reli ya Kisasa ya SGR, akisema uwekezaji huo umeonyesha kwa vitendo ubora na umakini wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha wananchi wanasafiri kwa usalama na uhakika.

Makonda amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Arusha, akieleza kuwa hivi karibuni Reli ya SGR iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma ilipata hitilafu njiani kuelekea Morogoro, na baadhi ya watu kutangaza kwenye mitandao ya kijamii kwamba treni hiyo imepata ajali.

Hata hivyo, alisema kutokana na ubunifu na teknolojia ya kisasa iliyoekezwa na Serikali, ndani ya masaa mawili na nusu tu treni nyingine ya mchongoko ililetwa na kuendelea na safari, na hakuna abiria hata mmoja aliyeshindwa kufika Dodoma au Dar es Salaam kwa njia ya SGR.

“Huu ndio ushahidi wa uongozi makini wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Enzi za nyuma behewa moja likidondoka, treni ilikuwa inasimama siku kadhaa; mvua ikinyesha kidogo reli inateleza na abiria wanakwama porini. Leo hii, ndani ya muda mfupi tu, tatizo linatatuliwa na safari zinaendelea kama kawaida,” alisema Makonda.

Makonda alisisitiza kuwa mafanikio hayo ni kielelezo cha Tanzania mpya yenye mifumo imara ya usafiri, inayotokana na dira ya maendeleo ya Rais Samia katika kuboresha miundombinu na huduma kwa wananchi.

0 0 votes
Article Rating
Subscribe
Notify of
0 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments

Trending

Exit mobile version