News
Riba ya Benki Kuu yabakia asilimia 5.75 robo ya pili 2026
Na Mwandishi wetu, News info
Benki Kuu ya Tanzania imeamua kuweka kiwango cha riba ya Benki kuu katika asilimia 5.75 kuanzia mwezi aprili, hatua inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5 na kupunguza athari za mgogoro wa kisiasa mashariki ya kati kwenye biashara na uwekezaji nchini, huku sekta ya zao la kahawa na korosho ikionyesha ukuaji thabiti.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Naibu Gavana wa Benki Kuu Dkt. Yamungu Kayandabila amesema kuwa uamuzi wa kudumisha riba thabiti unachangiwa na ukuaji imara wa uchumi, ambapo tanzania bara imefikia asilimia 6.2 na Zanzibar asilimia 6.7.
“Kamati iliamua Riba ya Benki kuu kubaki asilimia 5.75 kwa robo ya pili ya mwaka huu, kiwango hicho kilionekana ni sahihi kwa sasa kudhibiti mfumuko wa bei kubakia ndani ya lengo la asilimia 3-5”
“Kiwango hicho kitawezesha kupunguza athari za mgogoro wa kisiasa unaoendelea mashariki ya kati kwenye uchumi wa nchi yetu”
Amesema sekta za ujenzi, kilimo, utalii na huduma za fedha zimeendelea kuchangia ukuaji huo, huku mikopo kwa sekta binafsi ikiendelea kukua kwa wastani wa asilimia 22. aidha, uzalishaji wa zao la kahawa na korosho umeendelea kusaidia kuongeza mapato ya nje.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa umoja wa mabenki tanzania (TBA), Geofrey Mchangilla, ameipongeza Benki Kuu kwa usimamizi mzuri wa sera za fedha akisema hatua hizo zimeimarisha sekta ya benki na kuongeza utoaji wa mikopo.
Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya mabenki na serikali katika kulinda uthabiti wa kiuchumi na kuhakikisha viwango vya riba vinabaki himilivu, huku sekta ya kahawa na korosho ikiendelea kunufaika na utulivu wa bei katika soko la kimataifa.
