News

Sekta ya Afya Yapiga Hatua Kubwa, Serikali Yatakiwa Kuongeza Nguvu Vijijini

Published

on

Na Mwandishi wetu, News Info Online

Mkurugenzi Mkuu wa Health Africa Events, Dkt. Mshana Abdallah, amesema sekta ya afya nchini Tanzania imeendelea kuimarika kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, huku akieleza kuwa ongezeko la vituo vya afya, hospitali kubwa pamoja na kuanzishwa kwa teknolojia mpya za kitabibu ni miongoni mwa viashiria vya maendeleo hayo.

Akizungumza wakati wa utoaji wa Tuzo za Health Africa Awards, Dkt. Mshana alisema tuzo hizo ni jukwaa maalumu lililoandaliwa kwa lengo la kutambua na kuthamini juhudi, ubora na jitihada zinazofanywa na taasisi mbalimbali za afya, mashirika, wawekezaji pamoja na wadau wote wa sekta ya afya nchini.

Aliongeza kuwa kwa sasa sekta ya afya imekua kwa upana zaidi, huku maeneo yanayohitaji maboresho yakiwa ni machache sana. Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa serikali kuendelea kuweka mkazo katika kuboresha huduma za afya vijijini, hususan kuhakikisha upatikanaji wa madaktari na wataalamu wa afya katika vituo vilivyopo maeneo ya pembezoni.

Dkt. Mshana alisema utoaji wa tuzo hizo ni mara ya kwanza kufanyika, lakini utakuwa ni mwanzo wa safari endelevu ya kuhamasisha ubora katika sekta ya afya. “Niwapongeze washiriki wote waliopata tuzo leo, na tunatarajia kuona huduma bora zaidi za afya zikiendelea kutolewa nchini,” alisema.

Kwa upande wake, Dkt. Patric Shao, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Ajali kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na pia Mweka Hazina wa Chama cha Madaktari wa Dharura Tanzania (IMAT), alisema huduma za dharura ni muhimu kwa kiwango kikubwa kwa sababu dharura haziwezi kupangwa.

Alisisitiza umuhimu wa jamii kuwa na uelewa wa mbinu za awali za kuwahudumia wagonjwa wanaopata dharura za kiafya au ajali ili kusaidia kuokoa maisha.

Aliongeza kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili imekuwa ikiendesha mafunzo mbalimbali kwa watoa huduma za afya pamoja na makundi ya kijamii ili kuwajengea uwezo wa namna ya kuchukua hatua za haraka na sahihi wakati wa dharura za kiafya.

Naye Dkt. Nicas Mawazo, bingwa wa juu (super specialist) wa huduma za uzazi kwa njia ya IVF, alisema tuzo waliyoipata si ya bahati mbaya bali ni matokeo ya kazi kubwa wanayoifanya. “Watanzania wametuamini na wamethibitisha kuwa tunatoa huduma bora. Tutaendelea kutoa huduma zenye viwango vya juu zaidi kila siku,” alisema.

Dkt. Mawazo aliongeza kuwa taasisi yao ni jawabu kwa familia nyingi zilizokosa watoto, akisisitiza kuwa katika dunia ya sasa hakuna lisilowezekana. “Hakuna mwanaume asiyestahili kuitwa baba wala mwanamke kuitwa mama. Mafanikio yetu ni mengi, watu wengi wamepata faraja na watoto kupitia kliniki zetu,” alisema.

Kwa upande mwingine, Mkuu wa Idara ya Biashara, Masoko na Mawasiliano kutoka Taasisi ya Afya ya Aga Khan Tanzania Olayce Loatha alisema wamepokea kwa furaha kubwa tuzo ya mwaka 2025, akieleza kuwa ni ushuhuda kuwa Tanzania ina hospitali nyingi za umma na binafsi zinazotoa huduma bora za afya kwa viwango vya juu vya usalama na uangalizi.

Alisema tuzo hiyo ni motisha ya kuongeza juhudi, uwajibikaji na nguvu katika kuwahudumia Watanzania, akisisitiza lengo lao ni kuhakikisha hakuna mgonjwa anayeingia hospitalini hapo na kupoteza maisha. Pia alibainisha kuwa taasisi hiyo inaunga mkono jitihada za serikali katika kukuza utalii wa tiba (medical tourism), kwa kutoa huduma sawa na bora kwa Watanzania na wageni wanaofika nchini.

“Tunajivunia kuwa miongoni mwa hospitali zinazochangia kulifanya Taifa letu livutie katika huduma za kitabibu, na tutaendelea kuboresha huduma zetu kila wakati,” alisema.

0 0 votes
Article Rating
Subscribe
Notify of
0 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments

Trending

Exit mobile version