News
TotalEnergies wazindua kituo kipya cha mafuta Kimara
Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania imezindua rasmi kituo chake kipya cha kisasa cha mafuta, TotalEnergies Kimara Service Station, kilichopo Kimara, jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi huo umeashiria mwanzo wa huduma bora zaidi kwa wateja wa eneo hilo na maeneo ya jirani, kwa kuwapatia mafuta ya ubora wa juu na huduma za uhakika.
Kituo hicho kipya kinalenga kubadilisha kabisa uzoefu wa utoaji huduma za mafuta kwa wakazi wa Kimara na wasafiri, kikitoa bidhaa na huduma mbalimbali ikiwemo mafuta ya Excellium, huduma ya Fuel Card, mafuta laini ya ubora wa juu (lubricants) pamoja na gesi ya kupikia ya TotalEnergies.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo huku katika wiki ya huduma kwa wateja Afrika iliyoenda sambamba na kaulimbiu isemayo ‘Imani yako kwetu, nguvu yetu kila siku’ Mkurugenzi Mtendaji wa TotalEnergies Marketing Tanzania, Bw. Mamadou Ngom, alisema kuwa uzinduzi wa kituo hicho unaenda sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja Afrika 2025, ambayo inalenga kuthamini na kuimarisha uhusiano wa kampuni hiyo na wateja wake.
“Tunapozindua rasmi Kituo cha Huduma cha Kimara, tunasherehekea pia kuanza kwa Wiki ya Huduma kwa Wateja Afrika. Kaulimbiu ya mwaka huu ‘Your Trust, Our Everyday Energy’ inatukumbusha kuwa mafanikio yetu yanatokana na imani ya wateja wetu kwetu,” alisema Bw. Ngom.
Aidha, Bw. Ngom aliongeza kuwa ufunguzi wa kituo hicho ni uthibitisho wa dhamira ya TotalEnergies ya kusogeza huduma za nishati karibu zaidi na wananchi kupitia mpango wake wa Dealer-Owned-Dealer-Operated (DODO), ambao unalenga kupanua mtandao wa vituo vya mafuta nchini kote.
“Kituo cha Kimara ni alama ya uaminifu, ushirikiano na maendeleo misingi ambayo inatuongoza kila siku,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Bw. Godfrey Nyashage, ambaye ni mmiliki na msimamizi wa kituo hicho, alieleza furaha yake kuona ndoto yake ikitimia kwa kushirikiana na kampuni ya TotalEnergies.
“Niliamua kushirikiana na TotalEnergies kwa sababu naamini katika nguvu ya chapa yao na maadili wanayosimamia. Ushirikiano huu sio tu biashara, bali ni uhusiano wa kuaminiana na kujituma kutoa huduma bora kwa wateja wetu,” alisema Bw. Nyashage.
Aidha alisema ndani ya miaka mitatu ijayo anategemea kuwa na vituo zaidi ya vitatu ili aendelee kuwekeza ndani na hivyo kuweza kukuza uchumi wa Tanzania.
Kadhalika alisema mazingira ya uwekezaji kwa Tanzania ni mazuri kutokana na standard zake huku akiiomba serikali kuendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji yasiyo na usumbufu
Naye Juma Mohammed katibu wa umoja wa madereva bajaji-kwa Msuguli alishukuru ujio wa mradi huo kwani umewarahisishia upatikanaji wa mafuta kwa ukaribu hivyo wameondokana na adha ya kuzunguka kwa umbali mrefu kupata huduma hiyo
Uzinduzi wa TotalEnergies Kimara Service Station ni hatua muhimu katika safari ya kampuni hiyo ya kusogeza huduma za nishati bora karibu na wananchi, huku ikiendelea kupanua uwepo wake kote nchini Tanzania kupitia ushirikiano imara na mtazamo wa kumjali mteja.
