News
Wanawake 142 waanza mafunzo ya Female Future Programme Dar es Salaam
Na Mwandishi wetu, News info
Zaidi ya wanawake 142 wamepokelewa rasmi kushiriki toleo la 12 la programu ya mafunzo ya uongozi kwa wanawake, Female Future Programme (FFP), iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mafunzo hayo ya kiutendaji yameandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na Taasisi ya Usimamizi ya Afrika Mashariki na Kusini (ESAMI).
Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba-Doran amesema programu hiyo imekuwa na mchango mkubwa kwa zaidi ya wanawake 800 waliokwisha pata mafunzo kwa zaidi ya muongo mmoja, na sasa inaendeshwa katika nchi sita kwa ufadhili wa NHO, huku akiwahamasisha washiriki kushiriki kikamilifu safari ya miezi tisa ya mafunzo. Aidha, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ESAMI, Dkt. David Kalaba amesema jamii inahitaji wanawake viongozi wenye kujiamini na uwezo mkubwa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya haraka, akisisitiza umuhimu wa mtazamo wa kimataifa, kujifunza na kuendana na mabadiliko pamoja na uwezo wa kusimamia utofauti, kutatua migogoro na kutoa thamani kwa wateja.
Kwa upande wake, Meneja wa Upstream wa IFC, Bw. Sam Nganga aliyemwakilisha Meneja wa Nchi, Bi. Martine Valcin amesema taasisi hiyo inaendelea kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi katika ngazi za juu za uongozi ili kukuza ushirikishwaji, huku akiwahimiza washiriki kujisimamia na kutumia kikamilifu mafunzo hayo.
Katika hafla hiyo pia kulikuwa na mjadala wa jopo kuhusu wanawake katika uongozi uliowashirikisha wataalamu mbalimbali wa rasilimali watu na uongozi kutoka taasisi tofauti, ambapo ilisisitizwa kuwa kuchanganya uzoefu wa vizazi tofauti vya wanawake kazini huleta matokeo chanya pamoja na umuhimu wa kujifunza ujuzi mpya na kuimarisha mentorship baada ya mafunzo.
Washiriki wa kundi la 12 walihimizwa kujenga mitandao imara ya kitaaluma, huku taasisi na makampuni yakitakiwa kutambua upekee wa kila mwanamke badala ya kuwaona kama kundi moja.
Akihitimisha, Mjumbe wa Bodi ya ATE, Bw. Gasper Kikui amesema sekta isiyo rasmi bado ina changamoto nyingi za uongozi na kuwataka washiriki kuyachukulia mafunzo hayo kwa uzito ili kuleta mabadiliko chanya.
